Bahari ya Chumvi
Bahari ya Chumvi (kwa Kiebrania: יָם הַמֶּלַח yam ha-melaḥ "bahari ya chumvi"; kwa Kiarabu: ألبَحْر ألمَيّت al-bahrᵘ l-mayyit, "bahari ya mauti"; kwa Kiingereza: Dead Sea) ni ziwa lililoko kati ya nchi za Israel, Palestina na Yordani.
Ziwa liko ndani ya bonde la mto Yordani ambalo ni sehemu ya Bonde la Ufa la Afrika ya Mashariki. Eneo lake ni takriban km² 600.
Mwambao wa ziwa ni mahali pa chini kabisa kwenye nchi kavu ya dunia: uko mita 400 chini ya uwiano wa bahari.
Kwa sababu hiyo kuna joto kali linalosababisha maji mengi kugeuka mvuke na kuacha chumvi nyingi: kiasi cha chumvi ni mara tisa kulinganisha na chumvi katika maji ya Bahari ya Kati.
Kiasi hicho kikubwa cha chumvi kimezuia kuwepo kwa samaki ndani yake; uhai pekee ni aina za bakteria na algae.
Kiasi kikubwa cha chumvi kimesababisha densiti ya maji yake kuwa juu; hivyo binadamu huelea tu katika maji haya, bila ya kuhitaji jitihada yoyote.
Watalii hupenda kufika huko wakiogelea na kujipakia matope ya ziwa yanayosemekana kuwa na tabia za kuponya magonjwa ya ngozi.
Israel na Yordani zimeanzisha viwanda vinavyosafisha aina mbalimbali za chumvi kwa matumizi ya biashara.
Kwa jumla kiasi cha maji ziwani kimerudi nyuma kwa sababu mto Yordani, ambao ni mto wa pekee unaoingia humo, umehamishwa kwa shughuli za umwagiliaji.
Kuna sababu mbalimbali za kuelezea umaarufu wa bahari hii.
Kwanza, sifa yake imeenea kutokana na kutajwa sana kwenye Biblia, kitabu kitakatifu cha waumini Wakristo.
Pili, maji yake ina chumvi nyingi sana ambayo inafanya mtu kuelea anapoingia ndani. Yaani, hii ndiyo bahari pekee ambayo watalii huwakuta wenzao wakisoma gazeti majini bila kuzama. Chumvi yake ni kuanzia mara 8 ikilinganishwa na bahari zingine.
Uchunguzi makini unaonyesha kwamba chumvi kupita kiwango cha kawaida ndiyo sababu ya bahari hii kuwa na jina la kimaajazi, ‘ya kifo’. Hakuna uhai wa mimea wala wanyama unaopatikana katika bahari hiyo.
Lakini kuna bidhaa za maana zinazowavutia watalii: madini au matope ya Bahari hiyo yanasifika sana kwa sababu yana uwezo wa kutibu magonjwa mbalimbali.
Kama ilivyo desturi, watalii huzuru bahari hiyo na kuosha miili yao kwa kufaidika na madini hayo. Lakini si lazima mtu azuru Bahari ya Kifo ili apate matibabu kutokana na madini haya. Siku hizi kuna kampuni nyingi ambazo zinayauza kwa bei nafuu. Matope hayo yamebeba ioni ambazo hutoa uchafu na kemikali ambazo huharibu ngozi ya binadamu. Kulingana na mahitaji ya mtu binafsi, madini hayo yaweza kutumiwa peke yake ama pamoja na bidhaa nyingine kama vile mafuta ya ngozi na nywele.
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- https://www.researchgate.net/publication/6548248_A_facial_mask_comprising_Dead_Sea_mud
- https://floralbeautyspot.com/all-about-dead-sea-mud-mask/ Archived 23 Septemba 2020 at the Wayback Machine.
Makala hii kuhusu maeneo ya Asia bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Bahari ya Chumvi kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |