Nenda kwa yaliyomo

Ketusi (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nyota za kundinyota Ketusi (Cetus) katika sehemu yao angani
Ramani ya kundinyota Ketusi (Cetus) jinsi inavyoonekana kwa mtazamaji kwenye nusutufe ya kaskazini
Farisi (Perseus) jinsi alivyopigana na Ketusi akimlinda Andromeda - uchoraji kwenye chungu cha Ugiriki ya Kale


Ketusi (Cetus kwa Kilatini na Kiingereza) [1]. ni jina la kundinyota karibu na ikweta ya anga.

Mahali pake

Ketusi linaenea kwenye pande zote mbili za ikweta ya anga na iko pia karibu na mstari wa ekliptiki. Kundinyota jirani zake ni Samaki, (zamani Hutu, lat. Pisces), Kondoo (zamani Hamali, lat. Aries) na Nahari (Eridanus au mto wa angani).

Jina

Ketusi lilijulikana kwa jina hili kwa miaka mingi kati ya mabaharia Waswahili waliotumia nyota kutafuta njia baharini wakati wa usiku.[2]

Jina la Ketusi linatokana na Kiarabu قیطس qayṭus ambalo ni umbo la jina asilia la Kigiriki Κήτος Ketos (baadaye Cetus kwa tahajia ya Kilatini)..Wagiriki wa Kale walitumia jina hili kwa kutaja samaki kubwa sana pamoja na dubwana walioaminiwa kukaa baharini. Jina hili kwa umbo la Kilatini limeendelea kuwa jina la kisayansi kwa oda ya Cetacea (nyangumi).

Katika mitholojia ya Kigiriki Ketusi alikuwa dubwana aliyetake kumeza Andromeda kutokana na fitina na Poseidon mungu wa bahari. Shujaa Farisi (Perseus) aliingia kati akamwokoa Andromeda. Baadaye wote pamoja na mfalme Kifausi na malkia Cassiopeia waliinuliwa angani kama nyota [3]

Ketusi ni kati ya kundinyota lililotajwa tayari na Klaudio Ptolemaio katika karne ya 2 BK kwa jina Kassiopeia. Iko pia katika orodha ya kundinyota 88 ya Umoja wa kimataifa wa astronomia [4] kwa jina la Cetus. Kifupi chake rasmi kufuatana na UKIA ni 'Cet'.[5]

Nyota

Ketusi ni kundinyota kubwa lakini halina nyota angavu sana. Nyota angavu zaidi ni β Beta Ceti iliyoitwa Chura (lat. Diphda) na mabaharia Waswahili. Ina uangavu unaoonekana wa 2.0 ikiwa umbali wa miakanuru 96 kutoka Dunia.

Omikron Ceti inaitwa pia Mira (“ajabu”) kwa sababu ilikuwa nyota badilifu ya kwanza iliyotambuliwa kuwa vile na wanaastronomia wa Ulaya. [6] [7]

Jina la
(Bayer)
Namba ya
Flamsteed
Jina
(Ukia)
Mwangaza
unaoonekana
Umbali
(miakanuru)
Kundi la spektra
ο 68 Mira 2,0m hadi 10,1m 417 M7 III
β 16 Chura (Diphda), pia Deneb Kaitos 2,04m 96 K0 III
α 92 Menkar 2,54m 220 M1 IIIa
η 31 3,46m 118 K1 III
γ 86 Kaffaljidhma 3,47m 82 A2 + G5
τ 52 3,49m 11,9 G8 V
ι 8 3,56m 290 K1 III
ζ 55 Baten_Kaitos 3,76m 260 K0 III

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Cetus" katika lugha ya Kilatini ni " Ceti " na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Ceti, nk.
  2. ling. Knappert 1993
  3. ling. Allen, Star-Names and their Meanings uk, 117
  4. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  5. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy. 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R.
  6. Ridpath, Ian; Tirion, Wil (2001), Stars and Planets Guide, Princeton University Press, ISBN 0-691-08913-2, uk 114-116
  7. Omicron Ceti (Mira) – The Wonder Star, tovuti ya American Association of Variable Star Observers, iliangaliwa Agosti 2017

Marejeo

Marejeo

  • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 75 ff (online hapa kwenye archive.org)
  • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331
Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Ketusi (kundinyota) kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.