Nenda kwa yaliyomo

Daa-mkonga

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Daa-mkonga
Daa-mkonga (Amphiporus bimaculatus)
Daa-mkonga (Amphiporus bimaculatus)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia
Nusuhimaya: Eumetazoa
Faila ya juu: Lophotrochozoa
Faila: Nemertea
Schultze, 1851
Ngazi za chini

Ngeli 2, oda 3:

Daa-mkonga (kutoka kwa Kiing. proboscis worm) ni wanyama wadogo hadi wakubwa wa faila Nemertea. Wanyama hao wanafanana na daa wa kawaida lakini wanaweza kutoa mkonga kutoka katika kichwa chao ili kukamata mbuawa. Hutokea katika bahari zote, lakini spishi chache hutokea katika maji matamu au kwenye nchi kavu, hususa kwa mahali pa kitropiki na kinusutropiki. Spishi nyingi ni ndefu kiasi hadi sana, spishi moja ikifika zaidi ya m 50, lakini nyingine ni mm kadhaa tu. Mwili wao ni bapa kama utepe. Nyingi zina ruwaza za rangi za njano, machungwa, nyekundu na kijani.

Umio, tumbo na utumbo zimo kidogo chini ya mstari wa kati wa mwili, mkundu uko kwenye ncha ya mkia na mdomo uko chini ya ncha ya mbele. Juu ya utumbo ni rinkoseli (rhynchocoel), uwazi ambao mara nyingi hupita juu ya mstari wa kati na kuishia kidogo nyuma ya ncha ya nyuma ya mwili. Spishi zote zina mkonga ambao umo katika rinkoseli wakati haufanyi kazi, lakini hujitokeza juu ya mdomo ili kukamata mbuawa kwa sumu. Msuli unayoweza kurefuka sana kwenye nyuma ya rinkoseli huvuta mkonga wakati vizio limeisha. Spishi chache zilizo na miili minene na mifupi hujilisha kwa kuchuja na huwa na vinyonyaji kwenye ncha ya mbele na ya nyuma, ambazo huambatanisha nazo kwa kidusiwa.

Ubongo ni duara ya ganglioni nne, iliyowekeka kuzunguka rinkoseli karibu na ncha ya mbele ya mnyama. Angalau jozi moja ya neva kuu za upande wa chini huunganishwa kwenye ubongo na kupitia urefu wa mwili. Daa-mkonga wengi wana vipokezi mbalimbali vya kemikali na juu ya vichwa vyao baadhi ya spishi zina vikombe kadhaa vya pigimenti (oseli) ambavyo vinaweza kutambua nuru lakini haviwezi kuunda taswira. Daa-mkonga hupumua kupitia ngozi. Wana angalau mishipa miwili ya mbavu ambayo hujiunganisha kwenye ncha zao ili kuunda kitanzi, na hiyo na rinkoseli hujazwa na kiowevu kama “damu”. Hakuna moyo na mtiririko wa kiowevu hutegemea minyweo ya misuli katika mishipa na ukuta wa mwili. Ili kuchuja takataka ya metaboliki zilizoyeyuka seli za mwali hupachikwa katika sehemu ya mbele ya mishipa miwili ya kiowevu ya mbavu na kuondoa takataka hizo kupitia mtandao wa vibomba kwenda nje.

Daa-mkonga akila daa wa kawaida

Daa-mkonga wote husogea polepole wakitumia silio zao wa nje kuteleza juu ya nyuso kwenye njia ya ute, huku spishi kubwa zaidi zikitumia mawimbi ya misuli ili kutambaa na baadhi huogelea kwa miyumbo-yumbo juu na chini. Chache zinaishi katika bahari wazi huku nyingine zikipata au kujifanyia mahali pa kujificha kwenye sakafu. Takriban dazeni ya spishi hukaa katika maji matamu, haswa kwenye tropiki na nusutropiki, na dazeni nyingine ya spishi huishi kwenye nchi kavu katika maeneo manyevu yasiyo na joto sana. Daa-mkonga wengi wanakula wanyama kama anelidi, kombejozi na gegereka. Baadhi ya spishi za daa-mkonga ni walataka, na chache huishi kama mpangaji ndani ya uwazi wa joho wa moluska.