Nenda kwa yaliyomo

Uongo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kwa neno la kutaja kipindi cha miaka 10 tazama: mwongo
Pua ya Pinocchio inakua na kuwa ndefu kila akisema uwongo.

Uongo ni tamko lisilo kweli linalotolewa kwa makusudi. Mtu anayesema uwongo anajua au anahisi ya kwamba maneno yake si ya kweli lakini anataka msikilizaji wa maneno yake (au mpokeaji wa ujumbe wake) ayaamini kuwa kweli.

Mara nyingi uwongo hutumiwa kwa kusudi la kuficha kosa, aibu au tendo haramu. Kusudi lingine ni kujipatia faida au kuzuia hasara.

Uwongo hutazamwa kuwa tofauti na maneno yasiyo kweli lakini msemaji hajui kwamba si kweli au alikosea mwenyewe.

Aina za uwongo

[hariri | hariri chanzo]

Augustino wa Hippo alikuwa kati ya wataalamu wa kwanza waliofanyia uwongo utafiti. Katika kitabu chake "Kuhusu uwongo" ("De Mendacio") aliorodhesha aina nane za uwongo kama vile

  • Uwongo kuhusu mafundisho ya dini
  • Uwongo unaoleta hasara kwa mtu bila kumsaidia yeyote
  • Uwongo unaosababisha hasara kwa watu kadhaa na kuwasaidia wengine
  • Uwongo unaosimuliwa kwa furaha ya uwongo au kama mzaha
  • Uwongo unaotolewa kwa kumfurahisha mtu wakati wa maongezi
  • Uwongo usiomwudhi mtu lakini unaokoa uhai wa mtu
  • Uwongo usiomwudhi mtu na unaokoa heshima ya mtu
  • Uwongo usiomwudhi mtu na kumsaidia mtu

Hapa alitofautisha kati ya uwongo mzito (unaoleta hasara kwa mtu au uzima wa milele) na uwongo mwepesi (unaoleta faida kwa mtu bila kumwudhi yeyote). Lakini aliona kila aina ya uwongo kuwa dhambi kwa sababu unafanya watu wasiweze kuaminiana.