Nenda kwa yaliyomo

Samarkand

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Msikiti wa kihistoria wa Bibi Khanum.

Samarkand (kwa Kiuzbeki na Kirusi: Самарқанд; kwa Kiajemi: سمرقند) ni mji maarufu wa kihistoria katika Asia ya Kati. Ni mji wa pili kwa ukubwa katika Uzbekistan na mji mkuu wa Mkoa wa Samarkand.

Samarkand ilikuwa mapema mji muhimu ikiwa kituo kwenye barabara ya hariri (Silk Road) iliyounganisha China na nchi za Asia ya Magharibi na Ulaya.

Baada ya uenezi wa Uislamu ilikuwa kitovu cha Kiislamu kilichovuta wataalamu wengi.

Katika karne ya 14, ilikuwa mji mkuu wa milki ya Timur (Tamerlane) na ndiyo mahali pa kaburi lake linalojulikana kama "Gur-e Amir". Msikiti wa Bibi-Khanum bado ni mojawapo ya majengo maarufu zaidi ya mji.

Mwaka 2001, UNESCO iliingiza Samarkand katika orodha yake ya Urithi wa Dunia kama "Samarkand - Njiapanda ya Tamaduni".

Historia

[hariri | hariri chanzo]
Samarkand mnamo mwaka 1890.

Samarkand ni mojawapo ya miji mikongwe zaidi ulimwenguni. Hakuna uhakika iliundwa kwenye mwaka gani lakini kuna dalili za kwamba iliundwa mnamo karne ya 7-8 KK, ingawa kuna ushuhuda wa kiakiolojia ya makazi ya zamani zaidi[1].

Wakazi wa milki ya Uajemi ya Kale, Samarkand ilikuwa moja ya vituo vikuu vya ustaarabu wa Uajemi katika Asia ya Kati. Aleksander Mashuhuri aliiteka mji huo mnamo mwaka 329 KK.

Samarkand siku hizi.

Historia ya Enzi ya kati

[hariri | hariri chanzo]

Mwanzoni mwa karne ya 8, Samarkand ilitekwa na Waarabu Waislamu. Chini ya utawala wa Waabbasi, ilikuwa kituo cha kijeshi. Mahekalu ya Wazoroasta yalibomolewa, misikiti ilijengwa na wakazi wengi waligeukia Uislamu. Wakati ule teknolojia ya kutengeneza karatasi ilitambuliwa kwa njia ya wafungwa Wachina na kuenea katika himaya ya Waislamu[2], na kutoka hapo kwenda Ulaya.

Samarkand ilitekwa na Wamongolia chini ya Chingis Khan mnamo 1220 ikaendelea kuwa sehemu ya milki yao hadi mwaka 1370.

Mfanyabiashara wa Italia Marco Polo alipita huko akaandika ni "mji mkubwa sana na mzuri..." Wakati ule Samarkand ilikuwa pia kitovu kimojawapo cha Wakristo Wanestorio.

Mnamo 1370, Timur (Tamerlane) aliamua kuifanya Samarkand mji mkuu wa ufalme wake ulioenea kutoka Uhindi hadi Uturuki. Katika miaka 35 iliyofuata, alijenga mji mpya akaujaza mafundi kutoka sehemu zote alizoshinda. Timur alipata sifa kama mlinzi wa sanaa hiyo, na Samarkand ilikuwa na wakazi wapatao 150,000. [3]

Historia ya kisasa

[hariri | hariri chanzo]

Mnamo 1499, Waturuki Wauzbeki waliteka Samarkand. [3] Walipeleka mji mkuu kwenda Bukhara na Samarkand ilipungua. Tangu mwaka 1868 mji huo ulitawaliwa na Urusi. Sehemu ya Kirusi ya mji ilijengwa baadaye upande wa magharibi wa mji wa kale.

Mji huo baadaye ukawa mji mkuu wa Samarkand Oblast ya Turkestan ya Kirusi. Ulikuwa muhimu zaidi wakati reli ya ng'ambo ya Bahari ya Kaspi ilipofika huko mnamo mwaka 1888.

Chini ya utawala wa Wakomunisti ilikuwa mji mkuu wa Jamhuri ya Kisovyeti ya Kijamii ya Kiuzbeki mnamo 1925 kabla ya kubadilishwa na Tashkent mnamo 1930.

Baada ya kuporomoka kwa Umoja wa Kisovyeti ilikuwa mji wa Uzbekistan huru.

Asilimia kubwa wa wakazi bado hutumia lugha ya Kitajiki (aina ya Kiajemi) wakifuata Uislamu wa Kishia.

  1. Guidebook of history of Samarkand", ISBN 978-9943-01-139-7
  2. Quraishi S. 1989. A survey of the development of papermaking in Islamic Countries. Bookbinder. 29-36.
  3. 3.0 3.1 Columbia-Lippincott Gazeteer, p. 1657