Mercurius
Mercurius alikuwa mungu wa dini ya Roma ya Kale. Jina lake latokana na neno la Kilatini merx inayomaanisha "bidhaa".
Uhusiano na mitholojia ya Kigiriki
[hariri | hariri chanzo]Alitazamiwa na Waroma sawa na mungu Hermes katika mitholojia ya Kigiriki hivyo aliabudiwa kama mtume aliyebeba ujumbe kutoka mungu mmoja kwa wengine, pia kama mungu wa biashara, uchumi, mawasiliano na wezi.
Tabia zake
[hariri | hariri chanzo]Katika mitholojia alikuwa mwana wa mungu mkuu Jupiter na mungu wa kike Maia. Tabia yake kuu ilikuwa uwezo wa kuhama haraka hivyo sanamu zake mara nyingi zilionyesha viatu na kofia yenye bawa. Mwendo wake wa haraka ilisababisha pia kumwunganisha na sayari ya kwanza Utaridi iliyo na mwendo wa haraka kwa sababu obiti yake ni fupi kuliko sayari nyingine.
Matumizi ya jina lake katika lugha za Ulaya
[hariri | hariri chanzo]Kwa Kilatini na lugha za Ulaya sayari hii iliitwa pia Mercurius, kwa Kiingereza "Mercury". Mercury imekuwa pia jina la metali ya zebaki kwa Kiingereza kutokana na mwendo wake wakati inamwagika.
Alitazamiwa pia kama mungu mlinzi wa siku ya "Mercurii dies" yaani Jumatano inayoitwa kwa jina lake katika lugha za Kirumi hadi leo, kwa mfano kwa Kiitalia Mercoledì, kwa Kifaransa Mercredi, kwa Kihispania Miércoles na kwa Kiromania Miercuri.