Nenda kwa yaliyomo

Historia ya tarakilishi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Historia ya tarakilishi inasimulia hatua za maendeleo ya tarakilishi (kompyuta) toka aina ya kizamani hadi aina ya kisasa zaidi. Hatua hizo zinachukuliwa kama vizazi vya Tarakilishi.

Kimsingi tarakilishi ni kifaa chochote kinachomsaidia binadamu kufanya hesabu. Zipo tarakilishi za aina mbili: za kianalojia (za umakanika) na za kidijiti (za elektroniki). Za kwanza hazitumii umeme, na ndizo ambazo zilianza kabla ya tarakilishi za kidijiti (zinazotumia umeme).

Hatua kabla ya vizazi vya Tarakilishi

[hariri | hariri chanzo]
Mfupa wa ishango.

Tarakilishi za Analojia ni vifaa vinavyosaidia kufanya hesabu vikiendeshwa kwa mtangamano wa moja kwa moja na vidole. Mifano ya Tarakilishi hizi ni kama vile Fito za Kuhesabia, Fimbo za Hesabu, na kadhalika.

Calculi kilikuwa kifaa kitumikacho kuhifadhi hesabu. Vitu kama Pia, Tufe Mfinyanzi, na kadhalika vinafungwa kwenye kopo kuwakilisha hesabu pengine ya wanyama wafugwao au nafaka.

Suanpan (Namba zinazowakilishwa kwenye Abakusi hii ni 6,302,715,408)

Abakusi ni aina nyingine ya Tarakilishi analojia, ambayo ni kibao maalum chenye shanga zilizovikwa kwenye fito kinachotumika kusaidia hesabu za kujumlisha na kutoa.

Kila Tarakilishi, kwa namna tofautitofauti, inahimili kitendo cha Pembejeo, Mchakato, na Zao. Yaani, kila Tarakilishi inaweza kupokea data (habari), kufanya mchakato na kutoa majibu ya zile habari zilizochakatwa katika mtindo wa taarifa.

Kitendo Pembejeo-Mchakato-Zao (Input-Process-Output) cha Abakusi kwa kawaida kabisa ni tendo la kusogeza shanga mahali kupya (pembejeo), Kuhesabu zile shanga zilizojitenga na nyingine (mchakato), na kuziona shanga jinsi ambavyo zimejitenga na nyingine ni Zao.

Mifano mingine ya Tarakilishi analojia ambazo zilitengenezwa kitaalamu zaidi, ni kama vile Automata na Programmable cart, hizi zilitengenezwa na Shujaa wa Alexandria miaka ya 10 – 70 Baada ya Kristo (AD).

Planisphere ilivumbuliwa na Abū Rayhān al-Bīrūnī miaka ya 1000 Baada ya Kristo (AD).

Kulikuwa na Tarakilishi analojia ambazo ziliundwa kwa sababu ya kufanya hesabu za falaki, ni kama zifuatazo, Antikythera mechanism na astrolabe kutoka Ugiriki wa kale miaka ya 100150 Kabla ya Kristo.

Equatorium na Universal Latitude-independent Astrolabe zilivumbuliwa na Abū Ishāq Ibrāhīm al-Zarqālī mnamo 1015 baada ya Kristo.

Seti ya majedwali kokotozi ya John Napier kutoka miaka ya 1680

Astronomical Clock Tower ilivumbuliwa na Su Song miaka ya 1090 BK wakati wa kipindi cha utawala wa kinasaba wa mfalme Song.

John Napier alihitaji kufanya mahesabu mengi ya kuzidisha wakati akitengeneza Chati ya Logi ya kwanza. Katika kipindi hicho akavumbua Tarakilishi analojia iitwayo Napier’s Bones. Napier’s Bones ipo kama Abakusi lakini hii ilitumika kufanya hesabu za kuzidisha na kugawanya.

Rula Mtelezo

Rula Mtelezo (Slide rule) ilivumbuliwa mwaka 1620. Hii ni Tarakilishi analojia iwezeshayo hesabu za kuzidisha na kuganya zifanyike kwa wepesi na haraka zaidi ukilinganisha na ilivyokuwa hapo nyuma. Hapa namba halisi zinawakilishwa kama umbali au nafasi baina ya vituo viwili katika mstari mnyofu. Rula Mtelezo ilikua ikitumiwa na vizazi vya wahandisi na wataalamu wa hesabu mpaka kilipokuja kuvumbuliwa Kikokotoo cha Mfukoni.

Muonekano nyuma ya Pascal's calculator. Pascal alivumbua huu mtambo mwaka 1642.

Mwaka 1645, Blaise Pascal, msomi kutoka Ufaransa, alivumbua Kikokotoo analojia na kukipa jina Pascal’s Calculator au Pascaline. Hiki ni chombo cha kufanyia hesabu, ambacho alikitengeneza kwa ajili ya kumsaidia baba yake katika kazi za hesabu, lakini hakikuwa na sifa bora kama ilivyotakiwa.

Mnamo 1672, Gottfried Wilhelm von Leibniz alivumbua Kikokotoo analojia kiitwayo Stepped Reckoner. Pia ndie mvumbuzi wa Mche Duara wenye gia nyingi zilizopangiliwa kitaalamu ambao ulikuja kupata umaarufu kwa kutumika zaidi katika miundo ya Tarakilishi analojia zilizofuata. Stepped Reckoner ni maboresho ya Pascaline ambapo sasa ikawa inafanya hesabu za kuzidisha na kugawanya moja kwa moja.

Miaka ya 1820 Charles Xavier Thomas de Colmar alivumbua Kikokotoo analojia kiitwacho Thomas Arithmometer, ambacho kilizalishwa na kuuzwa kwa wingi zaidi. Thomas Arithmometer kilikuwa sehemu kubwa ya kazi ya Leibniz.

Mwaka 1903, Ryōichi Yazu wa Japani aliiweka dhahiri Yazu Arithmometer. Hiki ni Kikokotoo analojia kilichotumia Mche Duara mmoja wenye gia ishirini na mbili (22), ambacho kilifanya hesabu mchanganyo katika mpango wa namba wa kizio cha pili na wa kizio cha tano. Hizi hesabu ni mashuhuri kwa watumiaji wa Soroban (Abakusi ya Kijapani).

Kikokotoo Curta kinaweza pia kufanya hesabu za kuzidisha na kugawanya.

Vikokotoo analojia kama vile Addiator yenye kufanya hesabu za kizio cha kumi, Comptometer, Monroe, Curta na Addo-X zilitumika mpaka miaka ya 1970.

Kikokotoo cha mezani cha kwanza kabisa kilichotumia umeme kilikuwa cha Uingereza kilichoitwa ANITA MK.VII

Mwezi Juni 1963 Friden aliitambulisha Tarakilishi ya kazi-nne EC-130. Ilitumia transista katika muundo wake na ilikuwa na skrini ya inchi 15 yenye uwezo wa kuonesha mpaka tarakimu kumi na tatu (13).

Tarakilishi toleo EC-132 iliweza kufanya hesabu za Kipeo cha Pili pamoja na hesabu zitumiazo Namba Tegemezi zitumikazo katika hesabu za kinyume katika kuzidisha.

Mwaka 1965, Maabara za Wang zilitengeneza Kikokotoo cha mezani kilichoitwa LOCI-2. Kikokotoo hiki kilitumia transista katika muundo wake na kiliweza kuonesha mpaka tarakimu kumi katika skrini yake. LOCI-2 iliweza kufanya hesabu za Logi.

Teknolojia ya Panchi Kadi

[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1801 Joseph-Marie Jacquard alitengeneza Kitanda Cha Mfumi ambapo bombwe iliyokuwa ikifumwa iliongozwa na Panchi Kadi.

Mfululizo wa Kadi unaweza kubadilishwa bila kubadilisha mfumo mzima wa umakanika wa Kitanda Cha Mfumi. Hii ilikua ni hatua muhimu ya mafanikio katika uandishi wa programu.

Mtambo wa hesabu kutoka IBM utumiao panchi kadi, ulipigwa picha mwaka 1936

Charles Babbage mara nyingi anafikiriwa kama mwasisi wa vifaa vya Tarakilishi za kisasa. Mwanzoni mwa miaka ya 1810 Babbage alipata maono ya hesabu za namba na chati zitakazofanywa kimashine.

Kuifanya ndoto yake kuwa kweli, Babbage akabuni Kikokotoo cha kufanya hesabu za namba zenye mpaka nafasi za desimali nane (8).

Kutokana na mafanikio ya wazo lake hili, mwaka 1830 Babbage akaweka mpango wa kuunda machine ambayo ingetumia panchi kadi kuchakata hesabu za sayansi ya namba.

Machine hii ingeweza kutunza namba katika vizio maalum vya kumbukumbu, na kungekua na aina flani ya uongozi mwandamano. Hii inamaanisha kwamba utendaji kazi mmoja ungefanyika kabla ya mwingine kwa namna ambayo mtambo ungerudisha majibu pasipo kushindwa. Mtambo huu ukaja kujulikana kama Analytical Engine, ambayo ni uwakilishi wa kweli wa vifaa vya Tarakilishi za sasa.

Charles Babbage aliunda mtambo wa kwanza ujulikanao kwa jina la Difference Engine mwaka 1833. aliendelea na ubunifu wake hadi mwaka 1837 ndipo akaiunda Analytical Engine.

Analytical Engine ilikua ni Tarakilishi ya Madhumuni-ya-Ujumla yenye kuweza kufuata utaratibu wa mfuatano wa mambo ya kutekeleza, iliyotumia panchi kadi na injini ya mvuke kwa ajili ya nguvu ya uendeshaji.

Ada Lovelace (Augusta Ada Byron) mtoto wa mwinyi Byron wa London Uingereza, anaaminika kama mwasisi wa uandishi wa programu za Tarakilishi na anachukuliwa kama mtu mwenye kipaji halisi cha hesabu.

Ada Lovelace alianza kufanya kazi na Charles Babbage kama msaidizi wakati Babbage akiunda Analytical Engine. Katika kipindi chake cha kazi na Babbage, Ada Lovelace akawa mbunifu wa kwanza wa seti za maelekezo ya kihesabu ambayo lazima yafuatwe katika mpango imara (hasa na Tarakilishi) ili kutafuta ufumbuzi wa tatizo flani la hesabu.

Zaidi, katika kufanya kazi na Babbage, kulipelekea Ada Locelace kubashiri Tarakilishi za baadae ambazo sio tu zingefanya hesabu za namba, bali pia kuzifanyia kazi alama, ziwe za hesabu au la.

Mtambo ambao ulitumia sehemu kubwa ya muundo wa Difference Engine uliundwa mwaka 1843 na Per George Scheutz akiwa na mtoto wake wa kiume aitwae Edward. Mtambo huu uliuzwa kwa serikali za Uingereza na Marekani, ulitumika mahsusi kuzalisha chati za logi.

Mwaka 1909, muhasibu kutoka Dublin Ireland, Percy Ludgate, peke yake aliunda Tarakilishi ya umakanika yenye kuweza kutumia programu.

Mwishoni mwa miaka ya 1880, muamerika Herman Hollerith akabuni kifaa cha kutunzia data ambacho baadae kinaweza kusomwa na mtambo. Baada ya majaribio ya awali na mikanda ya karatasi kutofanikiwa, akaamua kutumia panchi Kadi.

Kuzitengeneza Panchi Kadi Herman Hollerith akabuni Mtambo wa Kuorodhesha (Tabulator) na mtambo uitwao Key Punch.

Tarakilishi analojia zilizoendelea

[hariri | hariri chanzo]

Kabla ya vita kuu ya pili ya Dunia Tarakilishi analojia za umakanika na umeme zilionekana kuwa ni kazi iliyo katika “hali ya ustadi”.

Tarakilishi analojia ziliweza kutumika katika tatuzi za matatizo magumu kwa kutumia Tabia mishabaha. Hii ni faida mojawapo dhidi ya Tarakilishi dijitali ambazo haziwezi.

Tarakilishi analojia za umakanika zilitumia hesabu za hali nyingine za asili, kama vile uhamisho wa nishati, momenta, na kadhalika kutengeneza idadi za kifanani (data).

Kwa mfano Tarakilishi iliyotumia maji kama idadi ya kifanani (data), ilikuwa ni Water Integrator iliyoundwa mwaka 1928.

Kwa kutumia mkondo na kizio cha nguvu ya umeme, Tarakilishi analojia za umeme ziliumba Hali za Asili kua kama idadi ya kifanani. Kwa mfano Mallock Machine ilioundwa mwaka 1941.

Tarakilishi Planimeter ilitumia umbali kama idadi ya kifanani.

Tofauti na Tarakilishi dijitali za kisasa, Tarakilishi analojia hazikuweza kubadilika kiurahisi kupokea mazingira mapya. Zilihitaji kufungwa upya waya kwa kutumia mikono ili kuzibadilisha kutoka kufanyia kazi tatizo moja kwenda lingine.

Mkokotoo wa dijitali ya ki-elektroniki wa mwanzoni

[hariri | hariri chanzo]

Enzi ya ukokotozi wa kisasa ilianza kabla, na wakati wa vita kuu ya pili ya Dunia.

Kwanza kabisa vifaa vya elektromakanika, kama vile rilei, vilitumika.

Mwezi wa kumi na moja mwaka 1937 George Stibitz alivumbua kikokotoo kilichotumia rilei kilichoitwa Model K. Hiki ndicho kikokotoo cha kwanza kufanya kazi kwa mfumo wa namba jozi. K inasimama kama Meza ya Jikoni ambapo ndipo alipokiungia kikokotoo hiki.

Hata hivyo, vifaa vya sakiti za elektroniki vikatumika mbadala ya vile vilivyolingana navyo vya elektromakanika, hivyo hesabu za dijitali zikachukua nafasi ya hesabu za analojia.

Mwaka 1936, jalada la Alan Turing lilithibisha kwa kiasi kikubwa kuwa kishawishi katika swala zima la ukokotozi na sayansi ya Tarakilishi.

Turing alitoa maana ya Tarakilishi ya kazi zote ambayo ingetekeleza maelekezo ya programu iliyotunzwa kwenye mkanda. Muundo huu ukaja kuitwa Mashine ya Turing.

Mashine ya Turing ilikuwa na hifadhi ndogo sana.

Tarakilishi za kisasa zinaitwa kama Turing kamilifu, ambapo ni kama kusema uwezo wake wa kutekeleza seti za maelekezo ya kihesabu upo sawa kabisa na Mashine ya kazi zote ya Turing.

Palikuwa na mikondo mitatu iliyoenda sambamba ya uundaji wa Tarakilishi enzi za kipindi cha vita kuu ya pili ya Dunia.

Ya kwanza ilikua kazi ya Wajerumani, Konrad Zuse, kifupi Z1 mwaka 1938.

Pili ilikua uundaji wa usiri wa Tarakilishi iitwayo Colossus, nchini Uingereza mwaka 1943.

Mkondo wa tatu ulikua ni uundaji wa Tarakilishi ziitwazo ENIAC na EDVAC. Tarakilishi hizi ziliundwa na Eckert pamoja na Mauchly. Tarakilishi hizi zilitangazwa kwa mapana.

Teknolojia hii ilipelekea [kupitia Turing na wengine] kuundwa kwa Tarakilishi elektroniki ya kwanza ya kibiashara nchini Marekani.

Tarakilishi ya kwanza Duniani kutunza programu ilikua inaitwa Manchester, jina la utani Mtoto. Iliundwa na Frederic C. Williams, Tom Kilburn na Geoff Tootill, katika Chuo Kikuu cha Manchester kiitwacho Victoria, na kuanza kutumia programu yake ya kwanza tarehe 21, mwezi wa sita mwaka 1948.

Leibniz alielezea mfumo wa namba jozi (kiambato kikuu cha Tarakilishi zote za kisasa), hata hivyo hadi miaka ya 1940, miundo mingi iliyofuatia (Ikiwamo mitambo alioiunda Charles Babbage miaka ya 1822, pia hata ENIAC ya mwaka 1945), ilitumia msingi wa mfumo wa namba desimali.

Pete kihesabio cha ENIAC kiliigiza utendaji kazi wa tairi ya tarakimu ya mtambo makanika wa kujumlishia.

Tarakilishi ya elektroniki

[hariri | hariri chanzo]

Tunaingiza Habari (Pembejeo), Tarakilishi inachakata kwa njia ya elektroniki kulingana na maelekezo yapatikanayo katika programu inayotumika kwa muda huo, na kutoa matokeo (Zao).

Tarakilishi za elektroniki zina uwezo wa kufanya kiwango kikubwa cha hesabu na mikokotoo kwa muda mchache.

Kwa kweli tunatumia Tarakilishi kuchakata Picha, Sauti, Maandishi, na vitu vingine ambavyo havipo katika jinsi ya namba. Lakini vyote hivi vinategemea msingi wa hesabu za namba. Michoro, Sauti, na kadhalika ni namba ambazo zimetafsiriwa ndani ya mtambo.

Katika Tarakilishi za dijitali namba hizi ni Moja (1) na Sifuri (0), zinazowakilisha hali kuu mbili za umeme, aidha umeme umewaka (1) au umeme umezima (0). Huu ndio mfumo wa namba jozi utumikao na vifaa vya dijitali.

Kwa maneno mengine kila Picha, kila Mlio, na kila andishi linakua na kanuni jozi husika. Uunganishaji usio na mwisho wa hizi Moja (1) na Sifuri (0) ndio unatengeneza maelekezo yanayopatikana kwenye programu.

Vizazi vya Tarakilishi

[hariri | hariri chanzo]

Kwa ujumla Tarakilishi zinaweza kuwekwa katika makundi manne ya hatua za kimaendeleo.

Kila kundi liliishia kwa kipindi cha muda flani, na kila kundi lilitupa Tarakilishi ambayo aidha ni mpya na iliyoboreshwa, au maboresho flani kwa Tarakilishi iliopo.

Kizazi cha Kwanza cha Tarakilishi

[hariri | hariri chanzo]

Kundi hili lilianza miaka ya 1940 hadi miaka ya 1950. Tarakilishi ya elektroniki ya kwanza ilikua inatumia Taa Ombwe katika muundo wake. Kutokana na Taa Ombwe Tarakilishi hizi zikawa zinatoa joto jingi.

Tarakilishi za kipindi hiki zilikua kubwa sana na changamani. Pia zilitumia kiasi kikubwa sana cha umeme.

Tarakilishi hizi zilifanya kazi pole pole sana na ziliweza kufanya kazi moja tu kwa muda. Hazikua zikitumia Mfumo tendaji. Gharama za awali na endeshaji zilikua ni kubwa.

ENIAC ilikuwa ni kifaa cha kwanza cha elektroniki ambacho ni Turing-kamilifu, ambayo ilifanya kokotozi za mwendo wa mitupo ya makombora angani kwa jeshi la Marekani

Tarakilishi ya kwanza ya elektroniki ya Madhumuni-ya-Ujumla iliitwa ENIAC (Electronic Numerical Integrator And Computer).

ENIAC ilikuwa na ukubwa wa mita za mraba 167, uzito wa tani 27, na ilitumia umeme wa kilowati 150. Ilikuwa na maelfu ya Taa Ombwe, dayodi fuwele, rilei, kikinzanishi, na kapasita katika muundo wake.

Tarakilishi ya kwanza ya elektroniki isiyo ya Madhumuni-ya-Ujumla iliitwa ABC (Attanasof-Berry Computer).

Tarakilishi nyingine za enzi hii zifananazo na hizi ni pamoja na Z3 za Ujerumani, Tarakilishi ziitwazo Colossus ambazo zilikua kumi, LEO, Harvard Mark1, na UNIVAC zote za Uingereza.

Upunguzaji ukubwa wa umbo

[hariri | hariri chanzo]

Tofauti na ENIAC iliyotumia mtindo wa mchakato sambamba, EDVAC (Electronic Discrete Variable Automatic Computer) ambayo ni mrithi wa ENIAC, ilitumia Bongo kuu kimoja. Muundo huu ulikua rahisi na ulitumika kufanikisha wimbi la upunguzaji ukubwa wa umbo.

Kizazi cha Pili cha Tarakilishi

[hariri | hariri chanzo]

Kundi hili ni la zile Tarakilishi zilizotumika miaka ya 1955 hadi 1960.

Kuanzia miaka ya 1955 na kuendelea, transista zilichukua nafasi ya Taa Ombwe katika muundo mzima wa Tarakilishi, hivyo Tarakilishi zikapungua ukubwa wa umbo, gharama za awali na endeshaji zikapungua ukilinganisha na kundi la kwanza.

Tarakilishi zikatumia umeme mdogo zaidi hivyo na joto likapungua pia.

Kasi ya utendaji kazi ikaongezeka zaidi ukilinganisha na Tarakilishi za Kizazi cha kwanza.

Diski za kutunzia data ziliweza kuhifadhi makumi ya mamilioni ya herufi na tarakimu.

Tarakilishi ya kwanza iliyotumia transista iliundwa katika Chuo Kikuu cha Manchester mwaka 1953.

Tarakilishi iliyopata umaarufu sana ambayo ilitumia transista katika muundo wake iliitwa IBM 1401.

Mwaka 1956, kampuni ya IBM (International Business Machine) iliunda diski ngumu ya kwanza iitwayo IBM 350 RAMAC.

Kizazi cha Tatu cha Tarakilishi

[hariri | hariri chanzo]

Miaka ya 1960 na kuendelea ilishuhudia uvumbuzi wa Sakiti changamano (IC) ambapo Jack St. Clair Kilby na Robert Noyce, kwa kutumia udongo wa silikoni (ambao ni Nusu-kipitishi cha umeme) waliwezesha vifaa vya elektroniki kama vile transista, dayodi, na kadhalika kufungamanishwa kwa idadi kubwa katika kisilikoni kimoja.

Sakiti changamano (IC) ikachukua nafasi ya transista katika muundo wa Tarakilishi, hivyo Tarakilishi zikazidi kupungua ukubwa wa umbo ukilinganisha na za kizazi kilichopita.

Kasi ya utendaji kazi ikazidi kuongezeka zaidi.

Tarakilishi zikatumia umeme mchache zaidi hivyo joto likapungua pia.

Sakiti changamano (IC) ni ndogo kwa umbo na zinatengenezeka kwa ufanisi zaidi. Kwa sababu hii Mikroprosesa ikavumbuliwa.

Utambulisho wa Sakiti Changamano kwenye Tarakilishi

[hariri | hariri chanzo]

Kitendo cha Tarakilishi kutumia Sakiti changamano (IC) kilikua cha taratibu, hivyo Tarakilishi za Kizazi cha Pili ziliendelea kutumika.

Kwanza zikaja Tarakilishi Dogo (mini computer) ambazo bado zilitegemea matumizi ya transista.

Kisha zikaja Tarakilishi Dogo chotara (hybrid mini computer) ambazo zilitumia transista na Sakiti changamano (IC) kwa pamoja. Mfano wa Tarakilishi hizi ni kutoka kampuni ya IBM, System/360.

IBM System/360 zilikua ni ndogo zaidi kiumbo na bei rahisi ukilinganisha na Tarakilishi za kundi la Kwanza na la Pili. Ambazo ziliitwa Kiunzikuu (Mainframe).

Kizazi cha Nne cha Tarakilishi

[hariri | hariri chanzo]

Hili ni kundi la Tarakilishi zilizotumika kuanzia miaka ya 1971 mpaka sasa.

Tarakilishi hizi zinatumia Mikroprosesa badala ya Sakiti changamano (IC) hivyo zimepungua zaidi ukubwa wa umbo.

Mikroprosesa ni mfungamanisho wa maelfu ya Sakiti changamano (IC) zilizotambulishwa kipindi cha Kizazi cha Tatu, katika kisilikoni kimoja.

Ujio wa Mikroprosesa ukazaa mabadiliko ya Mikrokompyuta, ambazo zikaja kujulikana kama Tarakilishi Binafsi.

Kizazi cha Kwanza cha Tarakilishi Binafsi

[hariri | hariri chanzo]

Tarakilishi hizi ni zile zilizokua zikitumika katikati ya miaka ya 1971 na 1976.

Mwanzoni Mikrokompyuta zilikua ni mkusanyiko wa ajabu, mara nyingi zilikuja katika mtindo wa vifaa. Kimsingi nyingi zilikua ni maboksi yenye taa na swichi nyingi.

Zilitumika kipekee na wahandisi na wapendeleaji walioelewa mfumo jozi.

Kizazi cha Pili cha Tarakilishi Binafsi

[hariri | hariri chanzo]

Hizi ni Tarakilishi zilizotumika kuanzia mwaka 1977 mpaka sasa.

Mikrokompyuta zakawa rahisi kuzitumia na kufanya idadi kubwa ya hadhira iweze kuzipata.

Kwa kufanana, zinakuja zikiwa na Kibao mbonyezo, Kipanya, na skrini. Au pia unaweza kuzifunga kwenye televisheni.

Tarakilishi hizi zinakimu uwakilishaji muono wa maandishi na namba kwenye skrini.

Kifupisho

[hariri | hariri chanzo]

Katika historia ya vifaa kokotozi,

Kizazi cha Tano cha Tarakilishi

[hariri | hariri chanzo]

Huu ni mradi ulioanzishwa mwaka 1982 na Wizara ya Viwanda na Biashara za Kimataifa ya Japani kutengeneza Tarakilishi ambayo iwe na uwezo kama wa Tarakilishikuu (Super Computer), na kutoa jukwaa kwa maendeleo ya baadaye ya Akili bandia. Ndipo mradi huu ukaitwa Mradi wa Mifumo ya Tarakilishi za Kizazi cha Tano.

Mradi huu ulilenga kuitengeneza Tarakilishi hiyo kwa kipindi cha miaka 10, ambapo baada ya hapo mradi ungefikirika kumalizika na uwekezaji ungeanzishwa katika mradi mpya wa “Kizazi cha Sita”.

Upo mgawanyiko wa maoni kuhusu matokeo yake; aidha mradi haukuwa na mafanikio au jambo hili lilikuwa mbele ya wakati wake.

Pale ambapo vizazi vya Tarakilishi vilivyopita vilizingatia kuongeza idadi ya elementi zenye mantiki kwenye Bongo kuu moja, Kizazi cha tano katika kipindi chake kiliaminika badala yake kugeukia uongezaji wa idadi ya Bongo kuu kwenye Tarakilishi moja ili kuongeza utendaji.

Kuzaliwa kwa Tarakilishi

[hariri | hariri chanzo]

Kabla ya miaka ya 1920, Tarakilishi walikuwa ni Makarani binadamu.ambao walifanya mikokotoo. Kawaida walikua chini ya uongozi wa Mwanafizikia.

Maelfu wengi wa Tarakirishi waliajiriwa maeneo ya biashara, serikalini, na idara za tafiti.

Wengi wa Tarakilishi walikua ni wanawake, na walitambulika wana digrii ya Kalkulasi. Baadhi walifanya hesabu za kifalaki kwa ajili ya kalenda.

Baada ya miaka ya 1920, msemo Mtambo kokotoaji ukamaanisha mtambo wowote ambao unafanya kazi ya Tarakilishi binadamu, hususani zile ambazo zinafuatana na taratibu za utendaji za tasnifu ya Church-Turing.

Tasnifu ya Church-Turing

[hariri | hariri chanzo]

Tasnifu inaeleza kwamba, mbinu ya hisabati inaleta matokeo pale ikiweza kuwekwa kama orodha ya maelekezo yanayoweza kufuatwa na Karani binadamu kwa penseli na karatasi, kwa muda wote unaohitajika, na pasipo ubunifu au utambuzi.

Mitambo ambayo ilikokotoa kwa kutumia thamani endelevu ilitambulika kama aina ya analojia.

Mitambo hii ya analojia ilitumia vyombo vya mitambo ambavyo viliwakilisha idadi za namba endelevu, kama vile pembe ya mzunguko wa mpini au utofauti kwenye nguvu ya umeme.

Vifaa vya mitambo ya dijitali, kwa kupingana na analojia, viliweza kuonyesha hali ya uthamani wa namba na kutunza kila tarakimu binafsi.

Vifaa vya mitambo ya dijitali vilitumia difference engines au rilei kabla ya uvumbuzi wa vifaa vya hifadhi ya ndani.

Msemo Mtambo kokotoaji taratibu ukaanza kupotea mwishoni mwa miaka ya 1940, na kubaki Tarakilishi pale ambapo mwanzo wa kishindo wa Mitambo dijitali ya elektroniki ulipozoeleka.

Tarakilishi hizi ziliweza kufanya ukokotoaji ambao awali ulifanywa na karani binadamu.

Kwa sababu thamani zinazotunzwa na mitambo ya dijitali hazikuwekewa mipaka na tabia asili kama vifaa vya analojia, Tarakilishi mantiki, kwa msingi wa vifaa vya dijitali, iliweza kufanya chochote ambacho kiliweza kuelezewa kama “makanika halisi.”

Mtambo wa nadharia wa Turing, uliobuniwa na Alan, ni kifaa cha kubuni kilichoongelewa kinadharia ili kusoma tabia za vifaa kama hivyo.