Nenda kwa yaliyomo

Hermann von Wissmann

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Hermann von Wissmann
Historia ya Tanzania
Coat of Arms of Tanzania
This article is part of a series
Uendo
Historia ya Zanzibar
Afrika Mashariki 1800-1845
Ukoloni
Afrika ya Mashariki ya Kijerumani
Mkataba wa Zanzibar-Helgoland
Mkwawa
Vita vya Maji Maji
Vita vikuu vya kwanza Afrika Mashariki
Tanganyika
Mapambano ya uhuru Tanganyika
Uhuru
Uhuru wa Tanganyika
Mapinduzi ya Zanzibar
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Julius Nyerere
Ujamaa
Tamko la Arusha
Vita vya Kagera
Ali Hassan Mwinyi
Benjamin Mkapa
Jakaya Kikwete
John Magufuli
Samia Suluhu Hassan

Tanzania Portal

Hermann von Wissmann (* 4 Septemba 1853 kwa jina kamili Hermann Wilhelm Leopold Ludwig Wissmann mjini Frankfurt (Oder); † 15 Juni 1905 katika Austria) alikuwa Mjerumani aliyejulikana kama mpelelezi wa Afrika, mwanajeshi na gavana wa pili wa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani kati ya 26 Aprili 1895 hadi 3 Desemba 1896. Aliongoza jeshi la Kijerumani lililokandamiza vita ya Abushiri mwaka 1889.

Mpelelezi wa Bonde la Kongo

[hariri | hariri chanzo]

Wissmann alisoma shule ya sekondari mjini Erfurt na baadaye akajiunga na jeshi la Prussia, baadaye katika jeshi la utemi wa Mecklenburg (Ujerumani ya kaskazini). 1874 alipat cheo cha luteni.

Kadi ya picha ya Tanga inayomwonyesha Wissmann
Meja von Wissmann, 1891

Mwaka 1881 aliomba likizo akajiunga na safari ya upelelezi wa Afrika na kupitia Luanda (Angola) alivuka bonde la mto Kongo. Alikutana na mfanyabiashara Tippu Tip akajiunga naye na kuendelea hadi pwani ya Bahari ya Hindi na 15 Novemba 1881 alifika Saadani. Safari hii ilimpatia sifa ya kuwa mzungu wa kwanza aliyefaulu kuvuka Afrika kutoka magharibi hadi mashariki.

Baada ya kurudi Ujerumani kupitia Zanzibar na Misri aliajiriwa na mfalme Leopold II wa Ubelgiji kwa safari nyingine ya upelelezi katika sehemu za kusini ya bonde la Kongo. Kupitia Malanje (Angola) alipita kwenye njia ya mto Lulua hadi kufikia mto Kasai. Njiani aliunda kituo cha kijeshi cha Luluaburg (Kananga). Kwa njia ya maboti waliingia katika mto Kongo na baada ya siku 50 walifila Léopoldville (leo: Kinshasa). Baadaye alirudi tena kwa safari nyingine alipeleleza njia nyingine kutoka Atlantiki hadi Msumbiji kupitia ziwa Tanganyika na ziwa Nyasa.

Wissmann alijiunga na vita dhidi ya Abushiri

[hariri | hariri chanzo]

1888 alirudi tena Ujerumani. Wakati huohuo vita ya Abushiri ilikuwa ilianza tayari ambako wenyeji wa pwani la Afrika ya Mashariki walipinga majaribio ya Shirika la Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki kushika utawala juu ya miji ya Waswahili kati ya Tanga na Lindi. Maafisa wa shirika waliuawa au walipaswa kukimbia na vituo vya Bagamoyo na Dar es Salaam pekee vilifaulu kujitetea kwa msaada wa wanajeshi wa manowari za Kijerumani. Hapo ilitokea azimo la serikali ya Ujerumani kuingilia kati. Wissmann aliombwa na serikali ya chansella Bismarck kuunda jeshi la kukandamiza upinzani wa wenyeji wa pwani.

Wissmann alipandishwa cheo kuwa kapteni akapewa cheo cha Mwakilishi wa Kaisari katika Afrika ya Mashariki. Bunge la Ujerumani liliambiwa ya kwamba upinzani ulisababishwa na wafanyabiashara ya watumwa likakubali kiasi cha mark milioni 2 kwa "vita ya kukomesha utumwa". Wissman aliajiri maafisa 21 na maafande 40 kutoka Ujerumani akaelekea Afrika. Njiani alipumzika Misri akawaajiri askari Wasudan 600 kutoka jeshi la Misri (walioachishwa kazi wakati ule kutokana na kupungukiwa kwa jeshi la Misri baada ya vita ya Mahdi). Baadaye askari 150 Wazulu waliajiriwa katika Msumbiji kama nyongeza. Jeshi hili lilijulikana kama "Wissmanntruppe" (kikosi cha Wissmann). Walipewa usaidizi na manowari za Kijerumani zilizokaa kwenye Bahari Hindi mbele ya pwani la Afrika ya Mashariki.

Kwa jumla vita ya Wissmann ilikuwa kazi nyepesi kwake maana askari zake walikuwa na silaha za moto kama bunduki za kisasa, bombomu na mizinga midogo wakati jeshi la wenyeji ilishika mikuki, pinde na gobori tu. Tarehe 8 Mei 1889 kikosi cha Wissmann kilitwaa boma la Abushiri karibu na Bagamoyo, baadaye miji ya Saadani, Pangani na Tanga. Abushiri alikamatwa na kunyongwa tar. 16 Desemba 1889. Mwenzake Bwana Heri alipaswa kujisalimisha akasamehewa na Wissmann. Menginevyo Wissmann aliua wafungwa wengi kwa kuwashtaki kama waasi dhidi ya amani ya serikali.

Gavana wa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani

[hariri | hariri chanzo]

Wissmann alirudi Ujerumani alipoandika kitabu na kuzunguka nchi akihotubia mikutano ya kusambaza wazo la kupanusha koloni za Ujerumani. Pia alikusanya pesa kwa ajili ya meli iliyokusudiwa kupelekwa Ziwa Viktoria Nyanza. 1893 alisafiri tena Afrika akaipeleka meli kwenda Ziwa Nyassa kwa sababu upinzani wa Wahehe chini ya Mkwawa ulizuia safari katika Tanganyika ya kati.

1895 aliitwa na serikali kuwa gavana wa pili wa koloni lakini Desemba 1896 alipaswa kujiuzulu kutokana na matatizo ya kiafya akawa mtumishi wa wizara ya koloni huko Berlin.

1899 alipumzika akaishi Austria alipokufa tarehe 15 Juni 1905.

Kumbukumbu zake

[hariri | hariri chanzo]
Makumbusho ya Hermann von Wissmann huko Bad Lauterberg, Ujerumani

Baada ya kifo chake alikumbukwa kama shujaa wa ukoloni wa Kijerumani na sanamu zake zilisimamishwa katika miji mbalimbali pamoja na Dar es Salaam mahali ambako sasa iko Sanamu ya Askari. Katika miji zaidi ya 20 barabara zilipewa jina lake.

Lakini alikuwa pia na wapinzani. Maafisa mbalimbali katika serikali walisikitika jinsi alivyowahi kuwaua Waafrika wengi hovyo wakati wa vita ya Abushiri na baadaye kwenye safari ya Ziwa Nyasa. Kinyume kuna watu waliosifa jitihada zake za kukomesha biashara ya watumwa katika Kongo.

Baada ya mwaka 2000 majadiliano katika nchi ya Ujerumani juu ya kasoro zake yalisababisha kubadilishwa jina kwa mitaa mingi iliyoendelea kuwa na jina lake.

Aliandika vitabu kadhaa vilivyosomwa sana katika nusu ya kwanza ya karne ya 20kama vile

  • Im Innern Afrikas. Die Erforschung des Kassai während der Jahre 1883, 1884 und 1885, Leipzig 1888
  • Unter deutscher Flagge quer durch Afrika von West nach Ost. Von 1880 bis 1883 ausgeführt von Paul Pogge und Hermann Wissmann, Berlin 1888.
  • Meine zweite Durchquerung Äquatorial-Afrikas vom Congo zum Zambesi während der Jahre 1886 und 1887, Frankfurt an der Oder 1890.
  • Afrika. Schilderungen und Rathschläge zur Vorbereitung für den Aufenthalt und Dienst in den Deutschen Schutzgebieten, Berlin 1895
  • In den Wildnissen Afrikas und Asiens. Jagderlebnisse von Hermann von Wissmann, Berlin 1901.

Viungo vya Nje

[hariri | hariri chanzo]
WikiMedia Commons
WikiMedia Commons