Benki kuu ya Kenya jana ilisema itaendelea na kiwango cha riba cha asilimia 7 kwa mikopo licha ya kupanda kwa bei za bidhaa nchini humo.
Gavana wa benki hiyo Bw. Patrick Njoroge aliyeendesha mkutano wa kamati ya sera ya fedha ya mjini Nairobi, amesema bei ya bidhaa hasa mafuta, ngano na mbolea imepanda sana kutokana na kukatika kwa usambazaji, kulikoongezeka wakati tayari kuna shinikizo la mfumuko wa bei duniani. Amesema hali kwenye soko la fedha inabadilika kutokana na mabadiliko ya sera za fedha yaliyofanywa kwenye nchi zilizoendelea.
Amesema mtazamo wa uchumi wa dunia kwa sasa hauna uhakika, hasa kutokana na mgogoro wa Russia na Ukraine ulioanza mwishoni mwa mwezi Februari, na kutokana na kutokuwa na uhakika kuhusu mwitikio wa kisera wa nchi zilizoendelea.