Usiku
Usiku ni kipindi cha siku kilichopo kati ya machweo na macheo na hasahasa kipindi cha giza kinachotokea baada ya machweo ambapo mwanga wa jua hauonekani tena angani hadi muda mfupi kabla ya macheo yaani kabla ya jua kuonekana juu ya upeo wa anga.
Kinyume chake ni mchana.
Kutokana na kupoteapotea kwa nuru ya jua, nyota zinaonekana usiku (pasipo mawingu).
Watu wengi pamoja na wanyama wengi hulala usiku, lakini kuna wanyama wengine wanaofanya shughuli zao usiku kama vile bundi, popo na wadudu wengi.
Nyakati za usiku
[hariri | hariri chanzo]Nyakati za mwanzo na mwisho wa usiku hutofautiana kati ya mahali na mahali duniani. Mstari unaofikiwa na mwanga wa jua unatembea juu ya uso wa dunia kutokana na mzunguko wa dunia kwenye mhimili wake.
Mwendo huu ndio sababu ya kugawiwa kwa uso wa dunia katika kanda muda.
Karibu na ikweta muda wa usiku ni masaa 12 sawa na muda wa mchana, lakini penginepo duniani, kadiri palipo mbali na ikweta kuelekea kaskazini au kusini, muda wa usiku hubadilika kila siku.
Usiku mrefu kabisa hutokea kwenye ncha za dunia ambako wala jua wala utusitusi havionekani angani kwa muda wa karibu miezi 3.
Katika tamaduni za binadamu usiku mara nyingi una maana mbaya kutokana na matatizo ya kutoona vema na hofu ya vitu visivyoonekana katika kipindi hicho.